Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Waislamu wa Texas wanasema kuwa; hotuba za kampeni za baadhi ya wanasiasa zimekuwa zikichochea chuki dhidi ya Uislamu, jambo ambalo linazidi kujitokeza katika maisha ya kila siku ya wananchi. Hali hiyo inaonekana katika mijadala kuhusu elimu na hata katika mawasiliano ya kijamii yanayofanyika madukani, masokoni, bustanini, vyuoni na katika shule za msingi.
Moja ya matukio yaliyotokana na hali hiyo lilitokea wakati wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Houston walipokuwa wakiswali, ambapo mtu mmoja aliwafuata ghafla na kuchoma nakala ya Qur'ani Tukufu mbele yao.
Katika matukio mengine, watu wamekuwa wakitukanwa na kushambuliwa kwa maneno mara kwa mara kwa sababu ya kuvaa mavazi yao ya Kiislamu au ya kitamaduni.
Baadhi ya wananchi, katika mahojiano mbalimbali, walisema kuwa hali hii ya chuki imewafanya wajisikie kutokuwa salama wanapotoka majumbani mwao.
Wengine walieleza kuwa wameamua kutumia kwa muda majina yasiyo ya Kiislamu hadi baada ya uchaguzi, kwa sababu wamekuwa walengwa wa vitisho na unyanyasaji kupitia mitandao.
Hivi karibuni pia, Waislamu walioshiriki katika mkutano rasmi wa Chama cha Republican cha Texas, wakiwemo baadhi ya wajumbe wa mkutano huo, walikabiliwa na mashambulizi ya maneno na kuambiwa ima waingie Ukristo au waondoke nchini.
Waislamu wa Texas wametoa wito wa kufanyika kwa mapitio ya kina ya sera za hivi karibuni za baadhi ya viongozi wa kisiasa, wakisema kuwa wanateseka kwa kiasi kikubwa kutokana na kampeni za chuki dhidi ya Uislamu zinazochochewa na ushawishi wa makundi yenye maslahi ya kisiasa yaliyo nyuma ya pazia.
Chanzo: The Guardian.
Maoni yako